FAWE ZANZIBAR , UN WOMEN ZINAVYOWAWEZESHA WANAWAKE KUFIKIA KIZAZI CHENYE HAKI NA USAWA KIUCHUMI.


NA MWANDISHI WETU,

FAWE Zanzibar, UN Women zinavyowawezesha Wanawake kufikia kizazi chenye usawa  kiuchumi.

KATIKA jitihada za kuhakikisha Tanzania inafanikisha utekelezaji  wa malengo manne ya kizazi chenye usawa wa kiuchumi, jukwaa la wanawake wanaelimu wa Afrika, Zanzibar (FAWE Zanzibar) inawezesha wanawake Zanzibar kukabiliana na vikwazo kiuchumi.

Kwa kushirikiana na UN women Tanzania, FAWE Zanzibar inachangia ufikiaji wa malengo hayo kupitia utekelezaji wa mpaango wa pamoja wa umoja wa mataifa wa kuharakisha maendeleo ya kiuchumi kwa wanawake Vijijini (JPRWEE) unalengo la kuhakikisha ustawi wa Wanawake Vijijini na haki zao.

Aidha, utekelezaji wa mpango huo unaenda sambamba na utoaji wa mafunzo kwa wanawake ili kusaidia kupata ujuzi wa biashara, elimu  ya kifedha, pamoja na fursa za kupata mikopo ili kuanzisha na kukuza biashara zao.

Miongoni mwa mafanikio  yaliyoelezwa na wanufaika wa mradi huo, ambao unatekelezwa mkoa wa kusini Unguja ni kuongezeka kwa ajira, hali iliyoboresha kipato cha kaya na kupunguza utegemezi kwa waume.

Walisema, mradi huo umewawezesha wanawake wengi kuanzisha biashara  ndogo ndogo, kama vile kukuza biashara za kilimo, ushonaji na uzalishaji wa bidhaa za nyumbani kama vile sabuni na mishumaa.

Si wanawake tu walionufaika na uwepo wa mradi huu, hata kwa wanaume pia mradi huu umebainika kuwa ufunguo wa kuwafikia haki na usawa wa kiuchumi.

Assa Hassan Khamis ni mwanakikundi cha upishi, SUBIRA INA MALIPO kutoka shehia ya Uzi Mkoa wa kusini Unguja, alisema'' mafanikio ninayojivunia ni kupata  mafunzo ya upishi ambayo yamenisaidia katika kujiajiri mimi mwenyewe na kumsaidia mke wangu majukumu ya kupika akiwa na tatizo''  alisema.

Nae, Mwakombo Nyange Shamata kutoka kikundi cha UROA SACCOS, alisema wamepata mikopo ambayo imewasaidia kununua vifaa vya ukulima wa mwani ambao ndio wanaoutegemea kwa kuendesha maisha yao ya kila siku.

''Tumepata mafanikio makubwa katika mradi huu kwani tumepata mikopo ambayo imetufanya tununue vifaa vya ukulima wa mwani ambao ndio rasilimali ya uchumi wetu'' alieleza mwakombo huku akitabasamu.

Kwa upande wa shida Hassan Mambo, kutoka kikundi cha TUPENDANE kilichopo  Uroa wilaya ya kati Unguja, alisema kupitia mafunzo ya usimamizi wa fedha , na kupanga matumizi mazuri , hali iliyosaidia biashara nyingi kukua.

'' Mradi umetusaidia sana sisi wanawake kufanya shughuli zetu za kiuchumi ikiwemo kuweka na kukopa jambo ambalo lilitusaidia kujikwamua na changamoto ya kifedha tunapopatwa na matatizo '' alisema mwanakikundi huo.

Licha ya juhudi kadhaa zinazochukuliwa, lakini Zanzibar bado inakabiliwa na changamoto ya soko la mwani.

''Serikali inasema kilo ya mwani inunuliwe kwa shilingi 1,000 lakini wanunuzi hununua kwa shilingi 700, hatupati chochote zaidi ya maumivu'' alisema Arabia Fauzi Pandu mwanakikundi cha mwani cha USALAMA WETU kutoka Jambiani wilaya ya Kusini Unguja.

Afisa Tathimini na ufuatiliaji FAWE Zanzibar, Shaban Suleiman alisema mradi una wawezesha wanawake wa vijijini kiuchumi ili kuona wanapata maendeleo ya kiuchumi katika maisha yao.

'' Tumewapatia elimu ya ujasiriamali na elimu ya biashara ili waweze  kufanya shughuli zao za kiuchumi katika kujikusanya kwa pamoja na tumewahamasisha  kuchukua mikopo Serikalini'' alisema Shaban.

Silivia Lanzarini, Afisa Ufuatiliaji na Matalam wa program kutoka UN women akitembelea wanufaika hao aliwashauri wajasiriamali wanawake kuweka akiba ya fedha kwenye vikundi vyao, ili waweze kupata mikopo zaidi itakayosaidia kutatua changamoto ndani ya vikundi vyao na jamii kwa inayowazunguka.

''Nimefurahi kukutana nanyi katika kuona mafanikio  na changamoto  zenu katika mradi huu, ni matumai yangu  mafanikio  muliyoyapata munayafurahia'' Silvia aliwaeleza huku akionesha kufurahishwa na juhudi zao.

Programu ya kizazi chenye usawa( 2021-2026) inajumuisha afua nne ikiwemo kuanzisha na kuendeleza vituo vya malezi na makuzi ya watoto, kuongeza uwekezaji katika  usambazaji maji, umeme na nishati mbadala yenye kukuza mazingira na matumizi ya teknolojia yenye gharama nafuu, kuongeza kazi zenye staha kwa kuendeleza biashara  na urasimishaji wa  biashara za wanawake, na kuboresha  upatikanaji na matumizi ya teknolojia nafuu na zinazofaa ili kuongeza  uwezo wa wanawake wa kuzalisha bidhaa zenye ushindani wa soko la ndani na nje.

No comments

Powered by Blogger.