WANDISHI WA HABARI WAPIKWA KUWA MABALOZI WAZURI KUELIMISHA JAMII USAWA WA KIJINSIA WANAWAKE NA UONGOZI


NA MARYAM NASSOR                                           CHAMA cha wandishi wa habari wanawake Zanzibar, (TAMWA ZNZ) kimewataka wandishi wa habari vijana kuwa mabalozi wazuri katika kushajihisha  usawa wa kijinsia katika uongozi kwa maendeleo ya nchi kwa ujumla.

Akifungua mafunzo ya siku tano , mkurugenzi wa chama hicho Dk Mzuri Issa Ali   alisema kuwa vijana  wa kiume wana nafasi kubwa ya kufanya uchechemuzi  kusaidia wanawake kuingia katika  maswali ya uongozi.

Alisema kuwa awamu hii vijana wa kiume wamepewa nafasi  kubwa, ukilinganisha na awamu iliyopita,  lengo la mradi huo ni  kuona  ongezeko kubwa la washiriki wanawake katika nafasi za uongozi.

“ Vijana wa kiume haikuwa bahati  mbaya kuchaguliwa katika mafunzo haya, bali tumefanya hivyo kwa kuwajenga kuwa mashujaa, mabalozi na wanaume wa mabadiliko katika kuhamasisha usawa wa kijinsia’’ alisema.

 Aidha DK Mzuri  alisema kuwa  wamechaguwa vijana wenye  taaluma mbali mbali  ikiwemo wandishi wa habari, wandaaji na waongozaji wa filamu ambao wanaamini watasaidia kuelimisha jamii kuhusu maswala ya usawa wa kijinsia na wanawake kushiriki katika vyombo vya maamuzi.

Nao baadhi ya wandishi wa habari  walioshiriki katika mafunzo hayo, wameishukuru TAMWA ZNZ, kwa kuwapa mafunzo hayo kwani yatawasaidia kuzidi kutoa elimu na   kuelimisha jamii na wanawake kuingia kwenye uongozi.

Nae mkufunzi Najjat Omar aliwataka washiriki wa mafunzo hayo,  kutumia takwimu katika kuandika Makala zao ili kuonesha hali halisi ya wanawake wangapi ambao wako katika uongozi .

Nae mshiriki Zurima Ramadhani kutoka radio asalam fm aliahidi kufanya kazi kwa  bidii  na  kuzidi kuelimisha  wanawake kuingia katika uongozi.

Chama cha wandishi wa habari wanawake Zanzibar TAMWA ZNZ imeandaa  mafunzo kwa wandishi wa habari vijana  25 Unguja na Pemba , ambapo  wanawake jumla ni 15 na wanaume 10 kwa kushirikiana na shirika na ( NED) la nchini marekani.

                           MWISHO

No comments

Powered by Blogger.