ELIMU NA MIUNDOMBINU RAFIKI INAHITAJIKA KATIKA KUKUZA USHIRIKI WA JINSIA ZOTE KATIKA MICHEZO- TUMBATU
NA MARIAM NASSOR.
Sheha wa Shehia ya Tumbatu Uvivini ndugu Ngwali Sheha
Haji, amesema miongoni mwa changamoto zinazopelekea kutokuwepo ushiriki sawa wa
kijinsia katika michezo ni pamoja na kukosekana kwa miundo mbinu rafiki na
skuli kutokua na muda maalum wa michezo kwa wanafunzi.
Sheha Ngwali amesisitiza kuwa
mila na desturi sio kikwazo kwani historia inaonesha kuwa kuna wanawake
mbalimbali kutoka kisiwani hapo ambao wamewahi kushiriki michezo na kuwa vinara
katika kisiwa hicho.
“Hapo zamani miaka ya 1973 wakati mimi ni
mwanafunzi kulikuwepo wanawake wanaoshiriki michezo na kuchukua medali nyingi
lakini ushiriki umepungua kutokana na changamoto za ukosefu wa mazingira rafiki
ya kushiriki michezo kwa watoto wa kike”, alisema Sheha Ngwali.
Nae Mwalimu mkuu msaidizi skuli ya Tumbatu
Msingi “A” ameeleza kuwa skuli hiyo ina mikakati ya kuwahamasisha watoto wa
kike kushiriki michezo hususan baada ya kukamilika viwanja rafiki vya michezo
kupitia mradi wa michezo kwa maendeleo.
Kwa upande wa wanafunzi wa kike wanaoshiriki
michezo hasa mpira wa mikono (netball) katika skuli hiyo wamesema kushiriki
kwao katika michezo kumewasaidia kuimarisha afya zao, kutembea sehemu
mbalimbali pamoja na kupata zawadi.
Pia wameiomba serikali na wadau mbali mbali
kuwaunga mkono kwa kuwasaidia vifaa mbalimbali vya michezo ikiwemo mipira, jezi
na vyenginevyo ili iwe rahisi kwa wao kushiriki katika michezo.
Katika muendelezo wa utekelezaji wa mradi wa
michezo kwa maendeleo, Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania Zanzibar
(TAMWA ZNZ) kimefanya ziara maalum pamoja na waandishi wa habari kutembelea
kisiwa cha Tumbatu kuangalia hali ya michezo katika kisiwa hicho.
Akizungumza katika ziara hiyo mkuu wa kitengo
cha mawasiliano TAMWA ZNZ Sophia Ngalapi amesema kazi kubwa ya TAMWA ZNZ ni
kutetea haki za wanawake na watoto pamoja na kukuza usawa wa kijinsia katika
kila sekta ndani ya jamii.


Post a Comment