FURSA ZA KUJIAJIRI KUPITIA MICHEZO KWA WATU WENYE ULEMAVU BADO HAZIJAWAFIKIA

 

 

NA MARYAM NASSOR

KATIBA ya Zanzibar ya mwaka 1984 kifungu cha 12 (1) kimefafanua kuwa watu wote ni sawa mbele ya sheria  na wanayo haki sawa bila ya ubaguzi wowote, kulindwa na kupatiwa haki sawa.

Lakini licha ya katiba kutamka wazi, lakini  ukiangalia suala la usawa kwenye michezo kwa watu wenye ulemavu  bado hawajapewa nafasi kutokana na mitazamo ya watu kuona hawana uwezo huo.

Mikataba yakimataifa na kikanda ibara ya (30) imeridhia  kushirikishwa kwenye michezo kwa watu wenye ulemavu, kwani imeonekana kuwa watu wenye ulemavu wanaachwa nyuma kushiriki katika michezo.

Akizungumza na mwandishi wa Makala haya,afisini kwako mjini Unguja, mchezaji wa timu ya watu wenye ualbino Abdillah Salum Shaame, amesema  fursa za kujiajiri  kupitia michezo bado hazijawafikia ipasavyo katika jumuiya zao.

Alisema kuwa, licha ya katiba kuwapa uhuru wa kushiriki katika michezo lakini hawashirikishi ipasavyo kama watu wengine waliyokuwa hawana ulemavu.

Aidha alisema kuwa, bado kuna watu hawataki kuamini kuwa ukimshirikisha mtu mwenye ulemavu basi, atashiriki na atashinda  na mifano ipo mingi.

 ‘’ Ni wakati wa jamii kuachana  na itikadi potofu ambazo zimepitwa na wakati,na badala yake watushirikishwe kwenye michezo kwani sasa michezo ni pesa na fursa za ajira ‘’ alisema.

Hapa aliiomba Serikali kama mdau nambari moja kuwajengea mazingira rafiki watu wenye ulemavu nao watumie fursa za michezo kujiajiri kwani ajira ni ngumu kupatikana.

 Nae, Hamad Ali mlemavu wa uziwi kutoka timu ya special Olympic Zanzibar (SOZ) akizungumza kwa lugha ya alama na ishara  kwa usaidizi wa mkalimani alisema kuwa anapenda sana kushiriki michezo.

Amesema kuwa, alishiriki mbio za olympiki nchini Ugiriki mwaka 2023 na kutokea mshindi wa kwanza na kurudi na medali nchini hivyo angependa kujiajiri kupitia michezo.

“ Licha ya kupenda michezo,lakini hatushirikishi sana kwenye michezo kama watu wengine waliyokuwa hawana ulemavu, watu huona sisi hatuna uwezo ‘’ alisema kwa masikitiko.

Aidha, aliwataka wazazi kuwaruhusu watoto wenye ulemavu kujiunga katika jumuiya hizo na wasiwafiche mayumbani, ili wafaidike na fursa za michezo.

Nae, Saada Hamad mwenyekiti wa timu ya special olympik ya Zanzibar, amesema timu za watu wenye ulemavu zinatengwa sana na wafadili ikilinganisha na timu za watu waliyokuwa hawana ulemavu.

Alisema kuwa, timu zao hazina vifaa vya kufanyia mazoezi wala kiwanja maalum vya mazoezi hivyo hupata wakati mgumu wakati wakijiandaa na mashindano ya kimataifa.

“ Timu zetu hazina bajeti kutoka Serikali wala hatuna viwanja vya kufanyia mazoezi wala vifaa vya mazoezi, hivyo tunapata  wakati mgumu wakati wa kujiandaa na mashindano ya kimataifa’’, alisema.

Aidhaa aiiomba Serikali na wadau wengine kuwasaidia katika ufadhili wa timu za watu wenye ulemavu kwani, mara nyingi timu zao hukosa ufadhili.

Ahmed  Khamis Iddi kapteni katika timu ya watu wenye  ulemavu wa mguu mmoja na mkono mmoja, amesema kuwa  wanapata msongo wa mawazo kwa kukaa ndani bila ya kushiriki katika kitu chochote ikiwemo michezo.

Amesema kuwa,hawana viwanja vya mazoezi kutokana na hali zao, wanafanya mazoezi katika viwanja vilivyokuwa na miti na mchanga mwingi  hivyo hupelekea kuumia misuli.

‘’ Tunakosa Amani kwa kukaa ndani kujifungia lakini tukikutana katika michezo tunapata matumaini na faraja na kujiona binadamu kama binadamu wengine na sisi tunatakakujiajiri kupita sekta ya michezo ‘’alisema.

Nae,Hassan Haji Silima katibu katika timu ya watu  wenye ulemavu wa mguu mmoja na mkono mmoja, amesema kuwa wana changamoto ya kiwanja cha kufanyia mazoezi na vifaa vya mazoezi  hawana.

 Hivyo, aliiomba Serikali kuwapa japo kile kiwanja cha nje cha uwanja wa Amani kwa ajili ya kufanyia mazoezi ili nao wawe na uhuru wa kukitumia.

 Aidha anakiri kuwa, michezo ni muhimu hasa kwa kuimarisha urafiki baina yao, na kutekeleza mkataba wa haki za watu wenye ulemavu.

Kanuni na sera ya michezo ya Zanzibar ya  mwaka 2018, imetamka wazi nia njemaa ya Serikali  katika kuhakikisha  uwepo wa usawa  wa jinsia katika michezo  lakini bado hawajafikiwa ipasavyo kundi la watu wenye ulemavu.

Sheria na.8 ya  mwaka 2022 ya watu wenye ulemavu kifungu  cha 28 (1) kinasema watu wenye ulemavu wanastahiki haki zote za msingi za binaadamu sawa na watu wengine .

Lakini katika kifungu cha 28 (f)  kinaeleza kuwa watu wenye ulemavu wanahaki ya kushiriki katika michezo na burudani kama watu wengine waliyokuwa hawana ulemavu.

Hija Mohamed Ramadhan mshauri katika maswala ya jinsia katika michezo katika mradi wa michezo kwa maendeleo unaofadhiliwa na shirika la Ujerumani nchini Tanzania (GIZ) umesema una lengo la kujenga viwanja saba vya michezo, vitatu Pemba na vinne Unguja hivyo katika viwanja hivyo iwaangalie na watu wenye ulemavu.

                     MWISHO

 

 

                                                                       

No comments

Powered by Blogger.