MTUHUMIWA WA KESI YA KUMUUWA MKEWE KWA KUKUSUDIA AENDELEA KUSOTA RUMANDE
NA MARYAM NASSOR ,
MTUHUMIWA wa kesi ya mauwaji, Khalfan Ali
Abdallah( 26) amepandishwa katika kizimba cha Mahkama Kuu Tunguu Zanzibar
,kwa tuhuma za kuua kwa makusudi chanzo kikitajwa ni wivu wa mapenzi.
Mara baada ya kufikishwa mahakamani hapo akitokea rumande na kusomewa
shitaka lake hilo na mwendesha Mashtaka wa Serikali kutoka ofisi ya Mkurugenzi
wa Mashtaka Zanzibar, Ali Amour Makame mshitakiwa huyo alikana shitaka hilo.
Awali, Mwendesha Mashtaka huyo alimueleza Jaji wa mahakama
kuu Zanzibar kuwa, kesi hiyo ni mpya na ipo kwa ajili ya Mshitakiwa kusomewa
shitaka lake hilo.
Mara baada ya kusomewa kosa lake, Mshitakiwa Khalfan Ali Abdallah
alikana kufanya kosa hilo la kumuua mkewe kwa makusudi.
“Muheshimiwa jaji, upelelezi wa kesi hii tayari umekamilika,
Mshitakiwa leo hii hana wakili na hajaieleza Mahakama yako kuwa atakuwa na
wakili au la, na kwa mujibu wa Sheria ya mwenendo wa Makosa ya Jinai ambayo ni
sheria namba 7 ya mwaka 2018, katika kifungu cha 198 na 199 , kosa
analoshitakiwa nalo ni kubwa na sheria hiyo inalazimisha mshitakiwa awe na
wakili atakaemuwakilisha, hivyo tunaomba kesi hii ihairishwe na kuipanga tarehe
nyengine ili kumpa muda mtuhumiwa kutafuta au kutafutiwa
wakili kwa ajili ya kumsimamia kesi yake” alidai Mwendesha Mashtaka huyo.
Baada ya maelezo hayo, Jaji wa mahakama kuu
Zanzibar Ali Mohamed alimuuliza mtuhumiwa huyo kuwa yuko
tayari kwa ajili ya kuhairishiwa kesi yake hiyo na kujibu ndio.
Kesi hiyo yenye namba 16/2024,kwa mara ya kwanza ilisomwa
mahakamani hapo juni 3 mwaka huu na kuhairishwa mpaka
tarehe 27 mwezi huu, kwa ajili ya kuteuliwa washauri wa mahkama na kutolewa
maelezo ya mashahidi mahakamani hapo.
Awali ilidaiwa mahakamani hapo na Mwendesha Mashtaka,
kuwa mstakiwa huyo anadaiwa kumuua kwa makusudi mkewe wa
ndoa kwa sababu ya wivu wa mapenzi.
Mshitakiwa huyo, alitenda kosa hilo, huko Bwejuu mkoa wa kusini
Unguja majira ya saa 10:00 usiku.
Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa, kutenda hivyo ni kosa
kinyume na kifungu cha 179 na 180 chini ya Sheria namba 6 cha
mwaka 2018 sheria za Zanzibar.
Jaji, alisema kuwa mtuhumiwa huyo kutokana na shitaka lake
hilo linalomkabili la kuua kwa makusudi akithibitika na kosa
hilo adhabu yake ni kunyongwa hadi kufa .
Kesi hiyo,imehairisha hadi
juni 27 mwaka huu kwa hatua ya kuteuliwa wasaidizi wa mahakama na kutolewa
maelezo ya awali.
MWISHO
Post a Comment