UDHALILISHAJI KWENYE MICHEZO , SUALA LILILO SAHAULIWA

 

 


NA MARYAM NASSOR, ZANZIBAR

WAANDISHI wa habari na wadau mbali mbali, wamekuwa wakielimisha jamii, kuhusiana na suala la udhalilishaji na ukatili wa kijinsia unaofanyika sehemu mbali mbali, ingawa wamekuwa wakiisahau sekta ya michezo.

 Katika michezo, kumekuwa kukifanyika udhalilishaji na ukatili wa kijinsia, lakini mara nyingi, umekuwa ukifumbiwa macho kwani watu wengi wamekuwa wakiinasibisha michezo na uhuni.

Lakini sio kweli  michezo ni afya na ndiyo  sekta ambayo inaongoza kwa kutoa ajira duniani, ikiwa  watashirikishwa vijana  ipasavyo.

Hivi karibuni, shirikisho la kandanda la nchini uhispania lilimshtaki Luis Rubiales, Mkurugenzi wa zamani wa shirikisho  hilo, kwa kosa la unyanyasaji wa kingono.

Ambapo ilikuwa ni kumpiga busu  hadharani, mchezaji wa timu ya wanawake  Jean Hermoso, alipokuwa akisherehekea ushindi wa kombe la dunia.

 Busu hilo, ambalo Hermoso na wachezaji wenzake walisema halikutakiwa na lilidhalilisha lilitokea  katika ushindi waliyoupata  dhidi ya  England baada ya kuwachapa  1-0  katika mashindano ya kombe la dunia.

 Wakati wa hafla  ya kukabidhiwa kombe la dunia, Rubeales alimshika  kichwa cha Hermoso, katikati ya mikono yake na kumpiga busu kwenye midomo yake.

 Jaji wa mahakama kuu nchini Hispania, alisema pia Rubeales, anakabiliwa  na shitaka  la kulazimisha kashfa  hiyona ikithibitika kosa hilo, hukumu yake ni mwaka mmoja jela.


 Hiyo, ilikuwa ni ulaya, lakini hata barani Afrika, bara lililojaa kila aina ya vipaji na wachezaji tumuangalie Caster Semanya.

 Semanya  ni mshindi wa mbio za mita 800 kutoka taifa la Afrika ya kusini mwenye miaka 28, anakabiliwa na shindikizo la kimataifa la Olympik (IAAF)  juu ya mpango wa kuwekewa  masharti  magumu ya viwango  vya juu vya testosterone.

Chini ya sheria za IAAF, mwanariadha wa kike mwenye viwango vya asili vya juu vya homoni za testosterone, anatakiwa kukimbia na wanaume au kushiriki mashindano ya watu waliyobadilishwa mpaka apate tiba ya kupunguza viwango hivyo.

Awali Semanya, aliagizwa na wakuu wa riadhaa, afanyiwe vipimo vya jinsia ,lakini hakuna matokeo yaliyotangazwa  rasmi kwa umma hadi sasa.

Zanzibar kama ilivyokuwa  sehemu nyingine duniani, kumekuwa kukitokea  vitendo vya udhalilishaji  kwenye michezo.

Ali Bakar Ali ( si jina lake halisi) akizungumza na mwandishi  wa makala haya alisema alishawahi kufanyiwa kitendo cha udhalilishaji  na kocha wake.

Alisema kuwa, makocha ndio uti wa mgongo wa klabu, ingawa baadhi yao, hawana maadili mazuri na kuharibu watoto.

“ Wakati nacheza katika timu za chini ya  umri wa miaka 15 kocha wangu, alinifanyia kitendo cha udhalilishaji,”alisema huku machozi yakimtoka.

Aidha alisema kuwa, lakini ni vigumu kuutambua udhalilishaji katika michezo kwani hata wachezaji kwa wachezaji, hawalizungumzii suala hilo.

“Sisi wachezaji kwa wachezaji, hatuna ujasiri wa kulizungumzia  suala hilo, kama tunafanyiwa udhalishaji na makocha au watu wengi kila mmoja anaweka siri kutokana na woga na kutojiamini kwake,’’anafafanua.




Aidha alisema kuwa, wakati mwingine kocha, anawataka wachezaji kimapenzi, ndio awapange kwenye kikosi na ukikataa unaweza usipate nafasi ya kucheza daima.

Haji Hamdu Nahoda  kocha wa timu ya  Warrious ya wanawake alisema, wachezaji wanakabiliwa  na vitendo vingi vya udhalilishaji na ukatili katika klabu zao.

Alisema kuwa, lakini wachezaji wengi hawana elimu ya udhalilishaji, licha ya kuwa  kesi za kwenye michezo haziingiliwi na Serikali kwa baadhi yao.

Mrajisi wa vyama vya michezo Zanzibar Abubakar Mohamed Lunda, alisema kuwa, wao ndio wenye jukumu la kusimamia  sheria na kanuni za michezo kwa hapa Zanzibar.

 Alisema kuwa, shirikisho la mpira wa miguu  (ZFF) wao ndio wanaoandaa na kutunga  miongozo na kuwapelekea  ofisi ya Mrajisi, kwa kuitekeleza.

Aidha alisema kuwa,  kesi yoyote  inayotokea ndani ya michezo inahukumiwa kulingana na sheria za  shirikisho la mpira wa miguu la Afrika (CAF) na lile na kimataifa la (FIFA).

Alisema ibara ya 58, ya katiba ya fifa inasema kesi yoyote inayotokea katika michezo basi haitakiwi kupelekwa katika mahakama za kawaida au kwa maana nyIngine Serikali, haitakiwi kuingilia kati.

Afisa programu kutoka chama cha wanasheria wanawake Zanzibar (ZAFELA)  Ruffea Juma, kwenye mradi wa michezo kwa maendeleo unaodhaminiwa na shirika la  Ujerumani (GIZ) alisema wao wataandaa miongozo kwa wachezaji, ambayo itatumika kama ni hamasa kwa wachezaji kuingia michezoni.

Mwandishi wa habari mwandamizi Hauwra Shamte, hivi karibuni alipokuwa  akiwapa mafunzo wandishi wa habari za michezo, aliwataka  kuripoti habari za usawa wa kijinsia, katika michezo.

Aidha alisema kuwa, wavulana na wasichana wanashindwa kufikia ndoto zao za kimichezo, kutokana na vikwazo mbali mbali, ikiwemo vitendo vya udhalilishaji na ukatili wa kijinsia katika michezo.

        MWISHO

 

No comments

Powered by Blogger.