TAMWA ZNZ, WAIKUMBUSHA SMZ KUHUSU SHERIA MPYA

 




NA MARYAM NASSOR

 WADAU wa habari nchini  wameiomba   Serikali ya Mapinduzi Zanzibar,  kukamilisha  mchakato wa marekebisho ya  sheria zilizotolewa maoni na wadau  ili kutoa mazingira rafiki  kwa waandishi  kutekeleza majukumu yao bila vikwazo  vyovyote.

 Akizungumza katika kongamano la siku ya habari, Mkurugenzi wa  chama cha wandishi wa habari  wanawake Zanzibar (TAMWA ZNZ) Dk Mzuri Issa Ali  huko katika ukumbi wa  kariakoo unguja.

Alisema , licha ya wadau  mbali mbali kutoa  na kuwasilisha  mapendekezo  yao kuhusu  mapungufu  yaliyopo kwenye   baadhi ya sheria za habari, lakini bado  utekelezaji wake umekuwa wa kusuasua  na kupelekea  mazingira magumu  ya utendaji kazi wa vyombo vya habari.

Alisema kuwa mchakato wa mabadiliko ya sheria za habari umekuwa kwa miaka mingi  lakini bado, sheria hizo  ambazo nyengine ni za muda mrefu zimekwama  kurekebishwa.

“ Sisi wengine  tangu tuko wandishi chipukizi tunazungumzia kupata  sheria hizi , tokea mwaka  2008, ni muda mrefu hivyo, tunahitaji kusimamia   jambo hili na hatimae tupate sheria  rafiki kwa waandishi wa habari’’ alisema.




Aidha alisema kuwa,   wadau wa habari wamefanya  mapitio ya sheria nane ,  ikiwemo ya usajili wa wakala wa habari , magazeti  na vitabu namba 5 ya mwaka 1988 iliyofanyiwa marekebisho na sheria no. 8 ya mwaka 1997,  sheria ya  tume utangazaji Zanzibr no. 7 ya mwaka 1997 iliyorekebishwa na sharia  no. 1 ya mwaka 2010 na kuwasilishwa kwa mamlaka husika.

Alisema kuwa, pia wamewahi kukutana na Rais na kumueleza kuhusu sheria hizi na waziri , lakini ipo haja ya kuonana  nao tena  ili tuone  hili linafikia pazuri.

“ Haitapendeza hata kidogo kuona huu mwaka unamaliza, na hatujajua hatma ya sheria hizi na kilio chetu cha muda mzuri kikiwa bado hakijapatiwa ufumbuzi” alisema.

 Katibu mtendaji  wa baraza la habari Tanzania (MCT) Ernest Sungura, akigusia  kuhusu uhuru wa  vyombo vya habari na mabadiliko ya tabianchi, alisema  vyombo vya habari  vitatekeleza kwa ufanisi wajibu wao, katika kulinda mazingira iwapo  wandishi watakuwa huru kutekeleza majukumu  yao bila ya hofu kisheria.

‘’ Kauli mbiu ya kimataifa mwaka huu ilikuwa  katika uhifadhi wa mazingira , lakini bila ya kuwa na sheria nzuri za habari hatuwezi kutekeleza  hayo tunayoyataka,’’ alisema.



 Aidha alivitaka vyombo vya habari kubuni  mbinu mpya za kukabiliana na changamoto za kiuchumi na kufikiria  njia ya kuendana na kasi ya mageuzi ya maswala ya kiteknolojia ili kulinda uhuru wao.

Akifafanua kuhusu mapendekezo ya  mchakato  wa mabadiliko ya sheria za habari  Zanzibar, Katibu Mtendaji Tume ya Utangazaji , Suleiman Salim alisema, tayari mapendekezo hayo yapo katika ofisi ya mwanasheria mkuu wa Serikali kwa ajili ya hatua zaidi.

 Alisema  mswada wa sheria za habari upo kwa mwanasheria mkuu na karibuni utakwenda  baraza la wawakilishi kama  mswada, hivyo tunawaomba waliokuweko kule wachangie vizuri ili uweze kupita.

“ Tayari Serikali  imeshakamilisha mchakato wa kuandaa sera mpya ya habari, na  ninawatoa hofu kuwa itazinduliwa hivi karibuni’’ alisema.

Maadhimisho ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari2024,  yameandaliwa na baraza la habari Tanzania Zanzibar ,( MCT ZNZ), chama cha wandishi wa habari wanawake ( TAMWA ZNZ) , jumuiya ya wandishi wa habari za maendeleo (WAHAMAZA)  na klabu ya waandishi  wa habari  Zanzibar ( Z P C)  kwa kushirikiana  na shirika la  Common weath Foundation  na kauli mbiu ilikuwa ni ‘’ UHURU WA VYOMBO VYA HABARI  NA MAGEUZI YA SERA NA SHERIA ZA HABARI ZANZIBAR’’

                         MWISHO

No comments

Powered by Blogger.