KUTOKUWEPO KWA MIFUMO YA KIELETRONIKI MAHAKAMANI KUNAVYO WAKOSESHA HAKI , WATHIRIKA WA KESI ZA UDHALILISHAJI.


      NA MARYAM NASSOR PEMBA,                   

 MATUKIO ya Udhalilishaji wa Watoto kama Ubakaji na Ulawiti si jambo geni visiwani Zanzibar.

Visiwani humu, haiwezi kupita siku bila ya kusikia kwenye vyombo vya habari vikitangaza kuhusu kesi za ubakaji na ulawiti .

Ikiwa si kusini, basi itakuwa kaskazini zimeripotiwa kutokana na kushamiri kwake, lakini vitendo hivyo utavisikia tu.

Kwa kweli, ni jambo la kuchukiza sana, kutokea katika visiwa vya Zanzibar, hasa kutokana na wananchi wanaoishi humu asilimia 99 ni waislamu.

Uislamu ni dini ambayo, inakataza vitendo viovu kama ubakaji na ulawiti ambavyo hata ibilisi mwenyewe hawezi kuvifanya.

Kwa mujibu wa taarifa ya Mwendesha Mashtaka Kutoka Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka Pemba, Ali Amour Makame alimweleza mwandishi wa makala hii kuwa mwaka  2021 jumla ya kesi 64  za Udhalilishaji ziliripotiwa  Afisini kwao.

Kwa mwaka 2022, jumla ya kesi 48  za Udhalilishaji ziliripotiwa, na kesi 26 ndizo zilizopatiwa hukumu na kesi 22 zilifutwa Mahakamani kutokana na kukosekana kwa ushahidi.

Wakati kwa mwaka  2023 mpaka novemba, kuna kesi 48 ambazo zimeripotiwa  na kesi 14 ndizo zilizopata hukumu.

Hadi novemba 2023, jumla ya kesi 7 ziliondolewa Mahakamani kutokana na sababu ya kukosekana  kwa ushahidi .

Na kesi sita, ziko tayari zinasubiri hukumu kutolewa na Hakimu wa Mahakama hiyo Maalumu ya makosa ya Udhalilishaji.

Mwendesha Mashtaka huyo, alifafanua zaidi kwa kueleza kuwa kesi nyingi hufutwa au kuondolewa Mahakamani kutokana na kukosa ushahidi.

Nilipomuliza wanalichukuliaje suala la kutokuwepo, Mazingira rafiki Mahakamani kwa kesi za watoto alinijibu bila kusita.

Alisema, Mahakamani zogo ni kubwa, uhuru wa kuzungumza kwa wathirika watoto bila ya kuwepo mtuhumiwa haupo.

Hivyo, “watoto wengi hushindwa kutowa ushahidi wao mbele ya Hakimu kutokana na woga wa kumuangalia mtuhumiwa.”

Aliendelea kusema, yeye binafsi ana kesi ambayo hawezi kuisahau hadi leo, ilitokea mwaka 2021  ya mtoto wa miaka mitano ambaye alishindwa kutoa ushahidi Mahakamani.

Alisema, “kesi hiyo ilitokea Gombani  Wilaya ya Chake Chake Mkoa wa Kusini Pemba, mtoto alishindwa kutoa ushahidi wake kutokana na hofu ya kumuona mtuhumiwa na kukumbuka vitisho vyake alivyompa.”

Hivyo aliongeza kwa kusema kuwa, Mahakama ilishindwa kupata ushahidi kutokana na Mazingira yalivyokuwa si rafiki kwa kesi za watoto hasa  kesi za Udhalilishaji.

Aliongeza mwendesha mashtaka huyo, “kwa mantiki hiyo, ikitokea mtoto ni mdogo na Mahakama hatumii video Conference, basi tunashindwa kupata ushahidi.”

Alieleza changamoto hiyo hupelekea mzazi kukata tamaa kwa kuona mwanawe  anavyoteseka  wakati wa kutoa ushahidi  kwa kukumbushiwa vidonda visivyo poa na kuamua kuiachia kesi.

Nae, Mkurugenzi wa Jumuiya ya Tumaini Jipya (TUJIPE), Tatu Abdallah Mselem alisema kesi nyingi za Udhalilishaji wa Watoto zinakosa ushahidi Mahakamani kutokana na hofu kwa watoto.

Alisema, watoto  bado hawajakomaa kiakili na anapotendewa Udhalilishaji anapata athari kisaikolojia.

“Ukimwambia mtoto atowe ushahidi na yule mtu aliyemtendea anamuona mbele yake, akikumbuka vitendo viovu anajawa na hofu na kushindwa kujielezea,” alieleza mkurugenzi huyo.

Aidha aliongeza katika harakati zao za kutoa elimu ya kesi za Udhalilishaji walikutana na mtu ambe mwanawe alifanjiyiwa Udhalilishaji ambapo alilalamika kesi yake kufutwa Mahakamni kwa sababu ya kutoandikwa kwa miaka ya muathirika wa Ubakaji ambae ni mwanawe.

Alimwambia mwandishi wa makala haya, “laiti Mahakama ingekuwa inatumia video conference basi kesi nyingi zingepata hukumu kama inavyostahili na mama yule angepata haki yake.”

Nae, Mrajisi wa Mahakama kuu Pemba, Faraji Shomari Juma, alikiri kuwepo kwa changamoto ya uendeshaji wa kesi za watoto kwa Mkoa wa kusini kutokana na tatizo la ushahidi kwenye kesi hizo.

Alisema, Mahakama hiyo kwasasa, haitumii mfumo wa kuendesha kesi kwa kutumia teknolojia (video conference) kutokana na kuwa na changamoto  ya mfumo kutofanya kazi vizuri.

Aliongeza, “licha ya changamoto hiyo, tayari tumeshapata mfadhili atakaye tusaidia kuweka sawa mfumo huo na kulitatua suala hilo karibuni.”

Tatu Abass Machano, ambae ni mshauri nasaha kituo cha Mkono kwa Mkono Chake Chake, alisema anaamini ushahidi unakosekana kutokana na wathirika kucheleweshwa kufika kituoni kwao kupata msaada wa kisaikolojia ili kumudu kufuatilia kesi zao.

Alifahamisha kuwa, wathirika wengi wa kesi za ubakaji na ulawiti ni watoto, hivyo wazazi huwachelewesha kuwapeleka jambo linalopelekea ushahidi kuharibika.

“Kwa hatua za awali kama ushahidi haukuonekana na daktari, hata ile michubuko haionekani vizuri kama mtoto kaingiliwa, hupelekea kukosekana kwa ushahidi na kama hakuna ushahidi hakuwezi kuwa na kesi,” alieleza mtaalam huyo.

Katika hatua nyingine aliongeza kuwa changamoto hiyo inachochewa zaidi na jamii kukosa uelewa wa kina kuhusu kesi za Udhalilishaji, kwani waathirika wengi wanapelekwa vituoni tayari kasha poteza ushahidi muhimu unaohitajika.

Nae, Mama wa mtoto aliyefanyiwa udhalilishaji Asha Bakar Juma (si jina lake halisi), alikiri kuwepo kwa tatizo hilo na kudai kuwa vitendo hivyo vinaonekana kuongezeka kila siku kutokana na hukumu kuwa ndogo kwa watendaji.

Alimwambia mwaandishi wa makala hii kwamba kesi ya mwanawe  iliondolewa  Mahakamani kutokana na kutoandikwa umri katika jalada la kesi tu jambo ambalo lilizua mkanganyiko na kupelekea mtoto wake kukosa haki yake.

Alisema, “Serikali ina nia thabiti katika kulitokomeza janga hili la Udhalilishaji lakini Mahakama inarejesha nyuma.”

Aliitaka Serikali kuweka Mazingira mazuri katika Mahakama Maalum  za Udhalilishaji ili haki siyo tu itendeke bali ionekane imetendeka kwa wote bila kujali hali ya mtu.

                           MWISHO.


No comments

Powered by Blogger.