Talaka si Suluhisho la migogoro, ipisheni mitihani ipite Safari iendelee.

 

Imeandikwa na Maryam Nassor - Zanzibar

Muda mrefu imekua ikiaminika na wanandoa wengi kuwa talaka ndiyo kimbilio la matatizo yote yanayowakumba katika maisha ya ndoa.

Katika  dini ya kiislamu, talaka ipo kisheria, ingawa maandiko matakatifu na yasio na shaka, ni haramu ambayo Muumba ameichukia.

Na wapo wanaoamini hata wakati wa kutolewa kwake ama kuandika, Imani inakubali kuwa, mbingu hutikisika, ni ishara kuwa si uamuzi sahihi sana.

Ijapo kuwa, maana ya ndoa ni mkataba wa hiari  ambao hufungwa kwa makubaliana baina ya mume na mke, ingawa pale inapofika  kuwa ndoa hiyo haina misingi ya kuendelea tena, basi hupelekea kutoka kwa talaka.

Mohamed Issa Ali mwanaharakati wa haki za watoto kisiwani Pemba, anashangaa kuona wanandoa kutowafikiria watoto ambao watakosa mapenzi na malezi ya wazazi wawili.

Na huwa hamufikirii hata kwa dakika chache tu, kuwa  lile janga la vitendo  vya udhalilishaji na ukatili wa kijinsia kwa watoto hao.

Utakuwa na uhakika gani kuwa, ule ulezi wa pande moja siku hizi unaitwaa ‘single mother’ utakavyooathiri malezi na makuzi ya watoto.

Asha Fadhil (36)  mkaazi wa Mahonda anasema yeye ni shuhuda wa mateso ya Watoto wanne wa kiume, waliyoachwa na wazazi wao baada ya kuachana na kupelekwa kwa bibi yao mzalia baba Mahonda.

Akizungumza na mwandishi wa Makala haya, alisema  Watoto hao mkubwa wao alikuwa ana umri wamiaka 16 na wapili alikuwa na miaka 13 na watatu alikuwa ana miaka 10 basi yule watatu alikuwa akimlawiti yule ndugu yao wa mwisho aliyekuwa na umri wa  miaka  sita.

Alisema kuwa, kila ikifika usiku alikuwa akimsikia akilia kwa uchungu, na yeye kama mzazi alikuwa akijiuliza huyu mtoto ana shida gani usiku.

Anasema, siku moja asubuhi aliamka na kuwasubiri wanaenda kucheza, akawaita na kuwauliza kwanini ndugu yao huwa analia kila ikifika usiku ndipo wakasema kuwa,huwa anavuliwa suruali na kaka ake anaelala nae na kumfanyia kitendo kibaya.

“Nilitokwa na machozi, kuwaona Watoto wale wanavyomtesa ndugu yao,  kumbe kaka zake walikuwa wanamlawiti’’ alisema kwa masikitiko.

Aidha, alisema kuwa chakushangaza Watoto wale walikuwa wanaishi na bibi na babu yao, lakini hakuna hata mmoja aliyekuwa anajali.

Ali Issa Kinole, Sheha wa shehia ya Mahonda alisema kuwa, baada ya kupata habari za manyanyaso ya Watoto hao, walitoa taarifa kwa watu wa ustawi wa jamii na kuja kuzungumza nao, ili wawashuhulikie Watoto wale vizuri.

 Mrajisi wa mahkama ya kadhi, Iddi Said Khamis  anasema  talaka za kiholela zinaweza kusababisha vitendo vya udhalilishaji  na ukatili wa kijinsia.

Alisema, takribani kesi nyingi za watoto unao wasikia kufanyiwa vitendo vya udhalilishaji basi,mara nyingi huwa wanaishi na mzazi mmoja inaweza kuwa wanaishi na mama pekee au baba na mama wa kambo.

Alisema kuwa, kwa sasa hali ni mbaya, talaka za kiholela  zimekuwa ni  nyingi, wanandoa hushindwa kustahamiliana na kuona suluhu pekee ni talaka.

Ingawa kwenye dini ya kiislamu, talaka imeruhusiwa  lakini ni jambo ambalo linamchukiza sana Muumba.

Aidha alisema kuwa,kitakwimu talaka zinazotolea kiholela zimekuwa zikiongezeka siku hadi siku.

Alisema, kwa mwaka 2023 jumla yakesi 909 zimeripotiwa katika mahkama ya kadhi wilaya ya Mwanakwerekwe Unguja pekee.

Na kesi 66 zimeripotiwa katika mahkama ya Mwera Unguja, huku kwa upande wa mahkama ya kadhi ya wilaya ya Makunduchi zilikuwa 60.

Aidha alisema kuwa, kwa upande wa Pemba kuliripotiwa kesi 119 kwa Mahkama ya kadhi ya wilaya ya Wete na kesi 45 kwa mahkama ya Konde.

Mrajisi huyo alisema kuwa, katika mahkama ya kadhi ya wilaya ya Chake chake ilionekana kuongoza kwa upande wa Pemba, ikiwa na kesi 126 za talaka.

Alieleza kuwa, kwa upande wa wilaya ya Mkoani , ziliripotiwa jumla ya kesi 64  na katika mahkama ya kadhi ya Kengeja zilifikishwa kesi 10.

Aidha, alisema kwa mwaka 2022 kulikuwa na kesi 416 zilizoripotiwa katika mahkama ya kadhi za wilaya Unguja na Pemba.

Alisema kuwa, ‘’utaona jinsi gani talaka zinavyotolewa kiholela, na kusahau kuwa zimeruhusiwa lakini kwa utaratibu maalum uliyowekwa’’,alisema.

Mratibu wa chama cha wandishi wa habari wanawake Tanzania, TAMWA Zanzibar Dk. Mzuri Issa Ali alisema, talaka siku zote sio nzuri kwa wanandoa, wanapaswa kukaa pamoja na kutafuta suluhu ya matatizo yao, mbali ya talaka.

Alisema kuwa, wazazi wanapotengana kwa sababu zozote zile, basi wanao umia zaidi ni watoto, kwani huwa ni wadogo na wanahitaji malezi na mapenzi ya wazazi wawili.

Aidha alisema kuwa, watoto hupitia kipindi kigumu katika maisha yao, pale ambapo wazazi hupeaana talaka.

Alisema kuwa, watoto waliyopitia vipindi vigumu vya kutengana kwa baba na mama, haawezi kusahau  katika maisha yao yote, shida na mateso waliyapata.

“Hivyo, tunashauri wazazi wakae pamoja kuzungumza tofauti zao, lakini si kuona suluhu pekee ni kupeana talaka,”alishauri.

Alifafanua kuwa, wao TAMWA- Zanzibar wataendelea kutoa elimu juu ya madhara yatokanayo na talaka, kupitia vyombo vya habari, ili kuwe na jamii bora ,ambayo inajikinga na vitendo vya udhalilishaji.

Fatma Ali Bakar, Mwanasheria kutoka  chama cha wanasheria  wanawake Zanzibar ‘ZAFELA’ alisema kuwa wanawake wanatakiwa kusoma ili kutimiza ndoto zao za kielimu.

Alisema kuwa, sababu moja wapo ya talaka ni kuwa wanawake wengi hukatishwa masomo na kupewa mume, hivyo bado wanakuwa hawajaandaliwa  kisaikolojia kuingia kwenye ndoa.

Nae, Mratibu wa maswala ya udhalilishaji shehia ya Mahonda Semeni Bundala, alisema kuwa kwa upande wa shehia hiyo, huwa wana toa ushauri kwa wana ndoa kuwa, wakae na kuzungumza tofauti zao.

Alisema kuwa, wanapo achana baba na mama basi watoto ndiyo, wanaoteseka na kupelekea kufanyiwa vitendo vya udhalilishaji.

Sheikh Nahoda  Haji wa msikiti wa Mahonda, alisema kuwa talaka ni jambo baya linalomchukiza mungu,  hivyo ni bora wazazi kuacha jazba kwa kutaka kuoneshana nani bora kuliko mwenzake.

Aidha alisema kuwa,  talaka huchangia vitendo vya udhalilishaji kwa watoto kwani, wazazi wakiwa mbali mbali kila mmoja huwa hana muda na watoto wao.

Nae, Askofu Stephen Aron wa kanisa la Mahonda, alisema kuwa katika dini yao talaka hairuhusiwi kutokana na kuwa wanaamini atakae muunganisha mungu, basi hakuna atakae mtenganisha.

Hivyo, jambo la talaka limekemewa vikali na dini yao, na hivyo wao hawaruhusu litokee, mpaka mmoja wao atakapo fariki.

Nao, baadhi ya wazazi waliyo wahi kuachwa na kuwaachia ulezi wa pekee yao, Bifarida Sudi wa Chuini mkoa wa mjini wa Magharibi alisema, kuwa talaka ni jambo baya sana, kwani watoto hukosa malezi ya pamoja ya baba na mama.

Alisema kuwa, yeye alipoachwa alikuwa anashinda ndani na kulia, alikuwa hajui la kufanya na watoto wadogo akiangalia hana kazi wala ndugu wa kumsaidia.

“Wazazi tunatakiwa kuzungumzia tofauti zao ili tupate suluhu, kwani watoto huteseka sana wakiishii na mzazi mmoja kwani hatuwezi kuwamalizia shida zao, hata kama mzazi atakuwa na kipato kizuri,’’ alisema.

Nae, Mzee Ali Faki Sungura alisema yeye alimuacha mkewe tu, kwasababu alikuwa haoni njia nyengine ya kupita zaidi ya talaka.

Alisema, baada ya kumuacha  talaka zote tatu ndipo alipokuja kutoka kwenye usingizi mzito aliyokuwa nao,na kukumbuuka ule msemo usemao” amekumbuka shuka kumesha kucha.

 

 

No comments

Powered by Blogger.