KAMATI YA MASWALA YA HABARI ZNZ, YAONGEZA KASI YA UFUATILIAJI MAREKEBISHO YA SHERIA.


 

 KAMATI ya wataalamu ya  maswala ya habari Zanzibar (ZAMECO) imekuwa mstari wa mbele katika harakati za kufuatilia mchakato wa marekebisho ya sheria za habari ikiwemo sheria ya utangazaji No. 7 ya 1997 ambayo ilifanyiwa marekebisho na sheria No. 1 ya mwaka 2010.

 Katika vikao mbali mbali ZAMECO ilitoa mapendekezo kuhusu marekebisho ya sheria hio kwa lengo la kupatikana kwa sheria mpya na rafiki kwa wandishi wa habari na vyombo vya habari nchini.

 Aidha, mnamo tarehe 9/4/2024 ZAMECO walifika katika Afisi za tume ya kurekebisha sheria  Zanzibar iliyopo Vuga kwa ajili ya kufuatilia hatua iliyofikiwa baada ya kupokea mapendekezo hayo mwezi wa Octoba mwaka 2023.

 Mratibu wa baraza la habari Tanzania (MCT) kwa upande wa Zanzibar Shifaa Said ameeleza kuwa, hatua hii ya ufuatiliaji imechukuliwa ili kuhakikisha mchakato wa kupatikana kwa rasimu ya sheria ya utangazaji  unakwenda vizuri na hatimae, sheria mpya itakayokidhi vigezo vya habari ipatikane.


Kwa upande wake, Salim Said mwandishi wa habari mkongwe amesisitiza kwamba vyombo vya habari havina lengo baya na Serikali, bali ni mdau wao muhimu katika kuleta maendeleo ya jamii, hivyo jitihada za ZAMECO na wengine katika kuendeleza maboresho ya sheria ya Utangazaji zinachukuliwa kama sehemu ya ushirikiano mzuri kati ya vyombo vya habari na Serikali.

 “ Vyombo vya habari havina lengo baya na Serikali, kwani sisi ni washirika wazuri na wenye lengo jema kwa jamii na Serikali kwa ujumla,kwa kuzingatia vyombo vya habari ni nguzo ya maendeleo ya uchumi” alisema.

Katibu wa tume ya kurekebisha sheria Zanzibar, Mussa  kombo Bakar aliwapongeza ZAMECO kwa jitihada wanazozichukuwa katika kutafuta maendeleo ya tasnia ya habari nchini na kubainisha kuwa mapendekezo waliyowasilisha yamepokelewa na kufanyiwa kazi.

 Nae, mkurugenzi wa Chama cha wandishi wa habari WanawakeTanzania ,Zanzibar (TAMWA ZNZ) Dkt Mzuri Issa ametoa shukrani kwa katibu na wafanyakazi wote wa Tume kwa ushirikiano wao katika mchakato huu wa kupata sheria mpya, huku akisisitiza umuhimu wa ushirikiano wao katika mchakato huu,kwa kuhakikisha upatikanaji wa sheria mpya kwa maslahi ya Zanzibar na wazanzibari wote.

Ni miaka 20 sasa wadau wa  maswala ya habari Zanzibar, wamekuwa wakipambania marekebisho ya sheria  mbali mbali za habari, ikiwemo sheria  ya usajili wa wakala wa habari, magazeti na vitabu No.5 ya mwaka 1988 iliyifanyiwa marekebisho na sheria No.8 ya mwaka 1997 na sheria  ya utangazaji No. 7 ya 1997 ambayo ilifanyiwa marekebisho na sheria No 1 ya 2010, ambayo oktoba mwaka jana tume ya kurekebisha sheria Zanzibzr ilipokea mapendekezo ya marekebisho ya sheria ya utangazaji kwa lengo la kupata sheria huru iliyokuwa rafiki kwa tasnia ya habari na jamii kwa ujumla.

                  MWISHO

              

 

No comments

Powered by Blogger.