RC KUSINI PEMBA, AITAKA MAHAKAMA KUENDANA NA KASI YA MABADILIKO

 

Na Is-haka Mohammed,Pemba.

Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba Mattar Zahor Massoud amesema maboresho ya mahakama hayataleta faida yeyote endapo wadau wengine hawataendana na kasi ya mabadiliko hayo, hivyo ni vyema taasisi hizo zifuate maboresho hayo hatua kwa hatua.

Mattar ameyasema hayo wakati akizungumza na mahakimu, mawakili, wanasheria na wananchi katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Sheria Zanzibar ambapo kwa upande wa Kisiwani Pemba maadhimisho hayo yamefanyika katika viwanja vya Tennis Chake Chake.

Alisema Mahakama imekuwa ikifanya maboresho makubwa ikiwemo kuimarisha utendaji wake, ujenzi wa majengo ya kisasa kwa ajili ya utoaji wa huduma zake jambo ambalo limeongeza weledi kwa Mahakama ikiwemo usikilizwaji wa  haraka wa mashauri mbali mbali yanayowafikia.






Kwa upande wake Jaji Mkaazi wa Mahakama Kuu Zanzibar Pemba Ibrahim Mzee Ibrahim alisema mahakama itaendelea kufanya kazi kwa weledi na uadilifu ili kufikia mafanikio makubwa katika malengo waliyojiwekea katika utoaji wa haki.

Alisema, wananchi wanapoitwa mahakamani  kuja kutowa ushahidi basi, wafanye hima  kwani wao ndio wanaosaidia mahakama kutenda haki ikiwemo kutoa ushahidi wa ukweli.

Aidha alisema, wao upande wa mahakama  wamejipanga kufanya kazi kwa  uwadilifu ,weledi na uwajibikaji  ili kila mtu apate haki yake kwa usawa bila ya kuangalia kesi ni ya nani.

Awali Wawawilishi wa Chama Cha Mawakili Zanzibar, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashkata wameeleza mipango yao mbali mbali pamoja na changamoto ambazo zinawakabili.

Maadhimisho hayo ya Siku ya Sheria Zanzibar ambao ni mwaka wa 12 tokea kuanza kuadhimishwa hapa Zanzibar,kunaashiria kuanza rasmi kwa mwaka mpya wa shughuli za mahakama hapa Visiwani.

 

No comments

Powered by Blogger.