KUELEKEA siku ya wanawake Duniani
NA MARYAM NASSOR
KUELEKEA siku ya wanawake Duniani, Uongozi wa serikali ya wanafunzi chuo cha utawala wa umma Zanzibar Ipa, kimeadhimisha siku hiyo, kwa kupanda miti katika skuli ya sekondari Jumbi na Tunguu wilaya ya magharibi B unguja, huku ikiwataka wanafunzi wa skuli hizo kuitunza miti hiyo.
Akizungumza na wanafunzi wa kike katika skuli hizo kwa nyakati tofauti Rais wa serikali ya wanafunzi chuo cha ipa, Nagila Abdalllah Ali alisema lengo la ziara hiyo, ni kuja kuwapa wanafunzi hao elimu ya mazingira, udhalilishaji na maswali ya uongozi ili waje kuwa viongozi bora wa baadae.
Aidha, aliwata wanafunzi wa kike kusoma kwa bidii na kufikia ndoto zao za kielimu ili waje kuwa viongozi bora wa baadae ndani ya familia zao na taifa kwa ujumla.
Alisema kuwa, wanawake ni kundi kubwa katika jamii hivyo, wana dhima kubwa ya kuelimika na kuielimisha jamii juu ya maswala ya udhalilishaji na matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii.
“Tumekuja hapa kwa lengo la kuwapa elimu ya mazingira na maswala mazima ya udhalilishaji na uongozi , ili muje kuwa viongozi wazuri wa baadae ‘’ alisema.
Nae, Afisa sheria wa wanawake kutoka ( zafela) Fatma Ali Bakari aliwataka wanafunzi wa kike kusoma kwa bidii na kujikinga na mimba za utotoni ili kufikia ndoto zao za kielimu.
Alisema kuwa,ni wajibu kwa kila mwanafunzi kusimamia masomo yake sambamba na kuacha tabia hatarishi ambazo zitaweza kumharibia malengo yake.
‘’ Munatakiwa kusoma kwa bidii na kuviepuka vishawishi ili kuepukana na ndoa za mapema na kufikia malengo yenu ya kielimi ili muje kuwa viongozi bora wa baadae” alisema.
Hivyo, aliwasisitiza wanafunzi hao kusoma kwa bidii na kuweza kujikinga na mimba za utotoni na kuacha tabia hatarishi.
Nae, mwenyekiti wa jumuiya ya vijana wenye taaluma Zanzibar Nadia Mwinyi Aboud aliwataka wanafunzi hao kuweza kujiongoza na kusimamia malengo yao ya kielimu.
Aidha aliwataka wanafunzi wakike kujua thamani zao kama wanawake ili wajuwe haki na fursa ambazo zimewazunguka ili waweze kunufaika nazo.
Nae, mwalim wa mazingira na ustawi wa jamii katika skuli ya Jumbi, Nassor Haji Juma aliwashukuru viongozi wa serikali ya wanafunzi chuo cha ipa na ugeni waliofuatana nao, na kuwataka isiwe mwisho waendelee kwenda kuwapa elimu.
Ziara hiyo ya siku moja ya kupanda miti na kutowa elimu kwa wanafunzi wa kike, kuelekea maadhimisho ya siku ya wanawake duniani inayoadhimishwa mach 8 ya kila mwaka yameandaliwa na uongozi wa ipa, wanasheria kutoka zafela na wasaidizi wa sheria Zanzibar.
Post a Comment