MTUHUMIWA KESI YA MAUWAJI ASOTA RUMANDE.
NA MARYAM NASSOR ,
MTUHUMIWA wa kesi ya kuuwa kwa makusudi,inayosikilizwa mahakama kuu Tunguu Zanzibar, inayomkabili kijana Omar Mahmoud Abdallah (36) mkaazi wa Jang’ombe Unguja,ameendelea kusota rumande,baada ya upande wa mashtaka kushindwa kukamilisha upelelezi wa shauri hilo kwa wakati.
Mara baada ya kufika mahakamani hapo, mtuhumiwa huyo akitokea rumande, mwendesha mashtaka kutoka ofisi ya mkurugenzi wa mashtaka Zanzibar Said Ali Said
Alimueleza, Jaji wa mahakama kuu Zanzibar kuwa, kesi iyo ipo kwa ajili ya kuanza kusikilizwa maelezo ya awali lakini bado upelelezi wa shauri hilo haujakamilika.
“Muheshimiwa jaji leo, kesi hii ipo kwa ajili ya kusikilizwa lakini bado hatujakamilisha upelelezi wa kesi na mashahidi, hivyo tunaomba utupangie tarehe nyengine kwa ajili ya kusikilizwa’’ alidai dpp huyo.
Baada ya maelezo hayo, Jaji wa mahakama kuu Zanzibar Ali Mohamed Ali aliwauliza mawakili wa upande wa utetezi uliokuwa ukiongozwa na mawakili wasomi Ali Rashid Ali na Elia Elisha kuwa wanakubaliana na ombi la upande wa mashtaka.
Wakili wasomi, walidai kuwa hawana pingamizi yoyote juu ya ombi hilo, ila wanataka upande wa mashtaka kujihimu kukamilisha maelezo ya kesi na mashahidi illi kesi hiyo ianze kusikilizwa.
“ Hatuna pingamizi na upande wa mashtaka ila tunataka, wajihimu kukamilisha maelezo ya kesi, ili mteja wetu ajuwe hatma yake mapema” walidai .
Jaji wa mahakama hiyo, aliuliza upande wa mashtaka kuwa ni lini, watakuwa wameshakamilisha maelezo ya kesi na mashahidi na kujibu hivi karibuni.
Jaji huyo, aliutaka upande wa mashtaka kuwa wanatakiwa kukamilisha maelezo ya kesi na mashahidi kwa wakati ili kesi hiyo ianze kusikilizwa.
Kwa mara ya kwanza shauri hilo, lilisomwa mahakamani hapo August 29 mwaka 2023 na kuhairishwa miezi mitatu mfululizo,kutokana na kutokamilika kwa upelelezi wa kesi hiyo.
Awali ilidaiwa mahakamani hapo na mwendesha mashtaka kutoka afisi ya mkurugenzi wa mashtka Zanzibar, kuwa mstakiwa huyo anadaiwa kumuua kwa makusudi kijana Seif Omar Salum.
Mshtakiwa huyo, alitenda kosa hilo, huko Jang’ombe wilaya ya mjini, mkoa wa mjini magharibi unguja majira ya saa 1:00 usiku.
Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa, kutenda hivyo ni kosa kinyume na kifungu cha 179 na 180 chini ya kifungu namba 6 cha mwaka 2018 sheria za Zanzibar.
Jaji huyo, aliutaka upande wa mashtaka kukamilisha upelelezi wa shauri hilo, ili kesi hiyo ianze kusikilizwa mahakamani hapo na kuihairisha kesi hiyo hadi machi 20 mwaka huu, kwa ajili ya kusikilizwa maelezo ya awali na mtuhumiwa kurejesha rumande.


Post a Comment