TAMWA ZNZ YATOA WITO WA ULINZI WA WATOTO KIPINDI CHA SIKUKUU YA EID EL-FITRI
Wakati tukielekea katika sherehe ya Sikukuu ya Eid-El-Fitri, Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA - ZNZ) kinatoa wito kwa wazazi, walezi na jamii kuchukua tahadhari za makusudi katika kulinda usalama na ustawi wa watoto kipindi chote cha sikukuu.
Kipindi
cha sikukuu huambatana na mikusanyiko na shughuli mbalimbali za kijamii ambazo
bila uangalizi wa karibu, zinaweza kuwaweka watoto katika hatari ya vitendo vya
ukatili na udhalilishaji wa kijinsia.
Karibu
kila mwaka wakati wa sherehe za Sikukuu ya Eid El Fitri au Eid El Adh-ha
huripotiwa matukio ya udhalilishaji kwa watoto katika maeneo mbali mbali ya
Zanzibar, ikiwemo kupotea kwa watoto, kubakwa, kulawitiwa, kutoroshwa na
matukio ya mengine ya aina hiyo.
Takwimu
zilizotolewa na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa
mwezi Januari 2026 zinaonesha ongezeko la vitendo vya udhalilishaji, katika
kipindi hicho, jumla ya matukio 113 yaliripotiwa, ambapo matukio 91, sawa na
asilimia 80.5, yaliwahusu watoto, ukilinganisha na mwezi Januari 2025, ambapo
jumla ya matukio 103 yaliripotiwa na kati yake matukio 87 (asilimia 84.5)
yalihusisha watoto.
Takwimu
hizi zinaashiria kuwa, vitendo vya udhalilishaji vimeshamiri na kutokana na
uzoefu wa miaka ya nyuma huongezeka zaidi wakati huu wa sikukuu kutokana na
watoto kuachiwa kutembea huru kwa wakati mrefu nje na ndani ya viwanja vya
kusherehekea.
TAMWA
- ZNZ inasisitiza kuwa, ni jukumu la pamoja kuhakikisha watoto hawatoki peke yao
kwenda sikukuuni, hivyo wazazi na walezi wanahimizwa kuwasimamia watoto wao kwa
karibu, kuongozana nao na kuhakikisha wanawanarejea nyumbani salama.
Aidha,
ni muhimu kuepuka kuwapa watoto jukumu la kuwasimamia au kuwaongoza watoto
wenzao, kwani nao bado wanahitaji uangalizi na ulinzi wa watu wazima, pamoja
kufuatilia mienendo isiyo ya kawaida na kutoa taarifa mapema kwa mamlaka
husika.
TAMWA
-ZNZ inaliomba , Jeshi la Polisi nchini kuimarisha ulinzi katika kipindi
hichi chote pamoja na matangazo ili kuwalinda watoto ambao wako kwenye kundi la
hatari kutekwa na kubakwa.
Hivyo,
TAMWA - Zanzibar inatoa wito kwa wazazi kuzungumza na watoto wao kuhusu usalama
wao, kuwajengea ujasiri wa kuripoti matukio yoyote ya vitisho au unyanyasaji,
na kuhakikisha wanakuwa katika uangalizi wa watu wanaoaminika wakati wote.
Vitendo ya udhalilishaji
vinazuilika endapo jamii itakuwa tayari kuelimishana na kukatazana maovu kwani
mhalifu hatoki mbali, bali hutoka ndani ya familia, majirani pamoja na jamii,
hivyo kila mmoja atimize wajibu wake katika kukataa udhalilishaji kwa wanawake
na watoto na kuhakikisha sikukuu ya Eid el-Fitri inakuwa ya furaha, amani na
usalama kwa wote.
Imetolewa na
kitengo cha habari
TAMWA Zanzibar
Post a Comment