DK MZURI ISSA AWAAGA RASMI WAANDISHI WA HABARI NA JAMII KWA UJUMLA,
NA MARYAM NASSOR
Dkt. Mzuri Issa amewataka waandishi wa habari, taasisi
mbalimbali pamoja na wanajamii kwa ujumla kumpa ushirikiano wa dhati Mkurugenzi
mpya wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania Zanzibar (TAMWA ZNZ).
Akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Chama
hicho Tunguu, Unguja, wakati wa hafla ya kuaga rasmi wanajamii, wadau na
waandishi wa habari baada ya kumaliza utumishi wake uliotukuka katika nafasi ya
Mkurugenzi wa TAMWA ZNZ, Dkt. Mzuri amesema anawashukuru wadau mbalimbali kwa
ushirikiano waliompa na kuwaomba kuendelea kutoa ushirikiano wa kutosha kwa
mkurugenzi mpya anayechukua nafasi hiyo.
Amesema kuwa, katika uongozi wake mafanikio kadhaa yamepatikana ikiwemo kuleta mabadiliko ya wanawake na Watoto nchini, kiuchumi na kijamii.
Akimtambulisha Mkurugenzi mpya wa Chama hicho, Dkt. Mzuri
alisema:
“Mimi mmenipa ushirikiano mzuri na mkubwa tangu mwaka 2007 hadi nilipomaliza
kuitumikia nafasi hii ya ukurugenzi mwaka 2025, hivyo naomba na huyu mkurugenzi
mpya mumpe ushirikiano huo kwa ajili ya taasisi yetu.”
Naye Mkurugenzi mpya wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Zanzibar, Nairat Abdullah Ali, amesema anafahamu kuwa uongozi ni dhamana kubwa aliyopewa na kuahidi kuutumikia kwa uaminifu.
Amesema katika uongozi wake ataendelea kupigania haki za
wanawake, kupinga sheria kandamizi za habari pamoja na kuimarisha uwajibikaji
na uwazi ndani ya taasisi hiyo.
“Napokea jukumu hili nikitambua kuwa taasisi hujengwa kwa
ushirikiano mzuri, na mimi milango yangu iko wazi muda wote,” alisema.
Aidha, amesema TAMWA ZNZ imejengwa juu ya misingi thabiti ya ukweli, uwajibikaji na ushirikiano mzuri wa waandishi wa habari, na kuahidi kuyaendeleza kwa mustakabali mzuri wa Chama hicho.
Kwa upande wao, baadhi ya waandishi wa habari waliohudhuria
hafla hiyo akiwemo Hatibu Suleiman wa gazeti la Habari Leo na
Huwaida Nassor wa Asalam FM, wamesema kuwa katika uongozi wa Dkt.
Mzuri, Chama hicho kilifanya kazi kubwa ya kuwajengea uwezo waandishi wengi wa
habari waliokuwa wachanga kitaaluma.
Wamesema Dkt. Mzuri alikuwa na ushirikiano mkubwa na
waandishi wa habari, na aliwajengea uwezo kwa kuwawezesha kifedha pamoja na
kuwapatia mafunzo mbalimbali.
Aidha, wameahidi kufanya kazi kwa karibu na Mkurugenzi mpya na kumpa ushirikiano mzuri kwa ajili ya ufanisi wa Chama hicho
Akisoma risala fupi kwa niaba ya wafanyakazi wa Chama
hicho, Afisa Zaina Mzee amesema wanamuaga Mkurugenzi huyo kwa heshima, si kwa
furaha, kwani alikuwa zaidi ya bosi — alikuwa mlezi na mama.
Amesema aliwajenga wafanyakazi wa taasisi hiyo kifikra na
kitaaluma kwa kuzingatia ubora, kufanya kazi kwa ushirikiano kama timu na
kuamini kuwa uongozi si cheo bali ni huduma.
Aidha, wamempongeza Mkurugenzi mpya kwa kuchaguliwa katika
nafasi hiyo na kuahidi kumpa ushirikiano mkubwa katika utekelezaji wa majukumu
yake.
Mwisho
Post a Comment