ZAFELA yaishauri Wizara ya Elimu kuweka askari kwenye fukwe kudhibiti utoro skulini

NA NUSRA SHAAABAN

MKURUGENZI wa Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA),Jamila Mahmoud Juma, ameishauri Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, kuweka askari wa doria fukweni ili kuwakamata watoto wanaozurura, hatua itakayosaidia kupunguza utoro na kuwarejesha skulini.

Akizungumza katika kikao maalum cha uthibitisho wa nyaraka za kumrejesha mtoto wa kike skulini kilichofanyika katika ukumbi wa Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA), Jamila alisema utaratibu huo utaongeza ufuatiliaji na kusaidia kupunguza idadi ya watoto wanaotoroka skuli na kuishia mitaani.

Alibainisha kuwa tatizo la utoro linaendelea kuongezeka licha ya jitihada mbalimbali zilizofanywa kurejesha watoto waliokuwa nje ya mfumo wa elimu.

Alieleza kuwa kwa mujibu wa utafiti wa mwaka 2018 wa Wizara ya Elimu, zaidi ya watoto 35,000 walikuwa nje ya mfumo wa elimu, wengine wakiwa wameacha skuli na baadhi yao hawajawahi kuandikishwa kabisa.

“ZAFELA kupitia mradi ulioanza mwaka 2023, imekuwa ikifuatilia changamoto hizi, ambapo hadi sasa wanafunzi 31 pekee ndio walioweza kurejeshwa skulini kupitia juhudi za pamoja na mashirika mengine ya kiraia.” Alisema Mkurugenzi Jamila.

Aliongeza kuwa wanafunzi wanaorejea skuli hukumbana na changamoto nyingi kama vile kukosa madarasa maalum au nafasi ya kufanya mitihani, hali inayosababisha baadhi yao kurejea mitaani.

Kwa upande mwingine, alisisitiza kuwa licha ya mradi huo kulenga zaidi watoto wa kike, pia watoto wa kiume wameathirika kwa kiwango kikubwa, jambo linalochochea ongezeko la ajira za utotoni kutokana na kukosa fursa ya elimu.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Ustawi wa Jamii, Hassan Ibrahim Suleiman, alisema kuwa mtoto wa kike anapokosa mazingira salama anakuwa hatarini kuathiriwa kimwili na kisaikolojia.

Alisema mtoto wa kike anatakiwa apate heshima, upendo na msaada kutoka kwa jamii na walimu ili apate ari  ya kusoma.

Kwa upande wake  Mratibu wa mradi wa MALALA FUND, Malhia Mabrouk Ali, alisema kuwa kati ya mwaka 2023 na 2024 waliwafikia watoto wa kike 3,572 kwa kutumia mbinu mbalimbali za elimu shirikishi kama michezo na mafunzo ya ufundi stadi.

Alibainisha kuwa waliunda kikundi cha “wasichana wa mabadiliko” kilichojumuisha wasichana 20 waliowahi kuacha skuli, ambao walirejea skuli na kujiunga na mafunzo kama ushonaji na uchoraji wa hina.

Akiwasilisha waraka wa nyaraka za kumrejesha mtoto wa kike skuli, Ofisa mabadiliko kutoka ZAFELA, Asya Mohd Juma, alisema kuwa sera ya elimu ya mwaka 2006 ina mapungufu yanayozuia watoto wa kike kubaki na kumaliza elimu.

“Ingawa marekebisho ya sera yameruhusu kurudi skuli kwa waliopata ujauzito, utekelezaji wake bado ni changamoto hasa kwa watoto wa vijijini.” Alisema Ofisa huyo.

Naye Afisa kutoka Wizara ya Elimu na mwanaharakati wa masuala ya wanawake, Ukhty Amina Salum Khalfan, alilaani matumizi ya adhabu kali dhidi ya wanafunzi, akisema si njia sahihi ya malezi.

“Watoto wanapaswa kulelewa kwa upendo na nidhamu, si kwa ukatili.” Alisema Ukhty Amina.

Kwa ujumla, kikao hicho kilisisitiza ushirikiano wa jamii, serikali na mashirika ya kiraia katika kuhakikisha watoto wote wanapata haki yao ya elimu kwa mazingira salama, rafiki na yenye usaidizi wa karibu.

 

No comments

Powered by Blogger.