Migogoro ya ndoa yazidi kuwaathiri watoto Zanzibar

NA NUSRA SHAABAN

ZANZIBAR inakabiliwa na ongezeko la talaka katika familia nyingi, hali inayowaathiri moja kwa moja watoto waliozaliwa ndani ya ndoa hizo.

Hayo yameibuliwa Katika mjadala wa wazi uliowakutanisha wanawake, wanaharakati, walimu na wataalamu wa sheria kuhusu ndoa na familia huko katika ukumbi wa Maji House Mjini Zanzibar.

Mwanasheria kutoka  Jumuiya ya Wanasheri Wanawake Zanzibar (ZAFELA), Mwanaisha Mustafa Makame,  alisema wanaume kutowajibika ni miongoni mwa sababu kubwa inayopelekea ongezeko la talaka visiwani humo.

Aliongeza kusema kuwa ripoti ya utekelezaji kutoka ZAFELA inaonesha kuwa Jumla ya malalamiko 1,934 yakiwemo malalamiko ya talaka,huduma,mirathi ,mgawanyo wa mali,idhini,cheti cha talaka,makaaazi ya watoto,kubaka na kulawitiwa yaliripotiwa kwa mwaka jana.

Alisema kati ya malalamiko hayo, malalamiko ya  ya talaka  kwa mwaka 2024, yalikuwa ni 834, ambayo yalipelekwa katika ngazi tofauti na mengine kupatiwa usuluhishaji.

Aliongeza kusema kuanzia mwaka wa 2025, malalamiko ya talaka yalipokelewa 344, ambapo mwezi wa Januari malalamiko ya talaka ni 72, mwezi Februari malalamiko ya talaka ni 78, mwezi Machi malalamiko ya talaka ni  68, mwezi  wa April malalamiko ya talaka ni 50 na mwezi Mei ni 76.


Kwa upande wake  Mkurugenzi wa ZAFELA, Jamila Mahmoud Juma alisema elimu ndio mpango mzima, ipo haja watoto wakaandaliwa tangu wadogo kujitambua kimaadili na hata kufundishwa na mapema wakiwa skulini jinsi ya kuishi maisha ya utuuzima.

“Watoto wanawasikiliza sana walimu wao, ni wakati sasa kwa kupitia mitaala iliyopo skulini, watoto kufundishwa adabu za ndoa na mapema”alisema Jamila.

Naye Ukhty Amina Salum Khalfan,ni   Afisa kutoka Wizara ya elimu ambaye pia ni mwanaharakati wa masuala ya wanawake katika Uislamu, alisema  jamii imeshindwa kujitambua na kuelewa dhamira ya ndoa, ambayo ni makubaliano ya hiari yanayohitaji uvumilivu, majukumu ya pamoja, na mshikamano.

Pamoja na hayo, Ukhty Amina alionya kuwa harakati za kuwawezesha wanawake, japo zina faida nyingi, zinaweza kutumiwa vibaya na kuwa kichocheo cha kuvunjika kwa ndoa.

Alieleza kuwa wanawake wanapopewa mamlaka bila malezi ya kimaadili na kiroho, wanaweza kutumia haki yao ya kudai talaka kwa misingi isiyo ya lazima.

Naye Omar Sheha Khamis Kadhi wa Mkoa wa Kusini Unguja  alieleza kuwa moja ya sababu zinazochochea talaka ni matumizi mabaya ya mitandao na ushawishi wa vipindi vya televisheni.

 Alieleza kuwa watoto na vijana wanajifunza kuhusu maisha ya ndoa kutoka kwenye tamthilia na filamu zisizo na maadili, wakidhani kuwa ndoa ni ugomvi, kutengana na matusi.

Aliongeza kuwa wazazi nao wanatelekeza majukumu yao kwa kutumia muda mwingi kwenye simu badala ya kujenga misingi ya familia.

“Jamii turudi katika sheria ya ndoa ya kiislamu kwa kuijua na kuifanyia kazi kwani, sheria ya ndoa ya kiislamu tayari imeshafafanua na kuweka wazi kila kitu, tatizo liliopo ni sisi wenyewe tunakiuka misingi iliyowekwa.” Alisema Sheikh Omar

Alitoa wito kwa viongozi wa dini na jamii kurudi katika misingi ya mafundisho ya ndoa na kusema  kuwa kuna haja ya kuzijadili upya aya za ndoa, kuzifafanua kwa muktadha wa kizazi cha sasa, na kuhakikisha kuwa waumini wanaelewa wajibu wao ndani ya ndoa.

 

No comments

Powered by Blogger.