ZAMECO YAPAZA SAUTI UPATIKANAJI WA SHERIA RAFIKI ZA HABARI BADO CHANGAMOTO.
NA MARYAM NASSOR
KAMATI ya Wataalamu wa Masuala ya Habari Zanzibar (ZAMECO) ikijumuisha (Klabu ya Waandishi wa Habari Zanzibar (ZPC), Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA -ZNZ), Baraza la Habari Tanzania (MCT), Jumuiya ya Waandishi wa Habari za Maendeleo Zanzibar (WAHAMAZA), pamoja Jukwaa la Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania, Zanzibar tunaungana na jamii ya kimataifa kuadhimisha Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani (World Press Freedom Day) ambayo huadhimishwa kila ifikapo tarehe 3 Mei kila mwaka.
Kwa Zanzibar kaulimbiu ya mwaka huu ni “Sheria nzuri ya Habari ni chachu ya uchaguzi ulio huru na wa haki”. Kaulimbiu hiyo yenye lengo la kuchochea majadiliano ya kitaifa kuhusu umuhimu wa upatikanaji wa sheria mpya na rafiki yenye kusimamia mazingira salama kwa waandishi wa habari hasa kuelekea kipindi cha uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu.
Katika kuadhimisha siku hii muhimu, ZAMECO inasisitiza maeneo makuu matatu ambayo ni: 1. Sheria Mpya ya Habari Zanzibar, ambayo itazingatia matakwa ya Katiba, Mikataba ya kikanda na kimataifa kuhusu uhuru wa kujieleza pamoja na maoni ya wadau wa habari waliyoyatoa katika mchakato wa uandaaji wa Muswada wa Sheria hiyo, sambamba na hayo Sheria hiyo itasaidia kujenga msingi wa uchaguzi ulio huru, wenye haki na uwazi.
2. Ulinzi kwa Waandishi wa habari wakati wa uchaguzi: Waandishi wa habari ni nguzo muhimu ya demokrasia. Wana haki ya kufanya kazi zao bila hofu wala vitisho, mashambulizi au unyanyasaji. ZAMECO inatoa wito kwa vyombo vya dola, vyama vya siasa, na wadau wote kuhakikisha waandishi wa habari wanawekewa ulinzi wa kutosha wakati wakitekeleza majukumu kipindi chote cha uchaguzi na baada.
3. Haki ya kuripoti bila kubaguliwa:Vyombo vya habari vina wajibu wa kuwafikia wananchi kwa usawa. ZAMECO inapinga vikali aina zote za ubaguzi kwa misingi ya itikadi, asili ya chombo au mtazamo wa mhariri/mwandishi ikiwamo kuwapo kwa kadi maalum zinazotolewa na Tume ya Uchaguzi, tunashauri kuwa kadi/vitambulisho vitolewe kwa kila mwandishi mwenye sifa za kuwa mwandishi na anayetarajia kuripoti wakati wa uchaguzi kwani huo ndio utawala bora, hivyo tunatoa wito kwa Tume ya Uchaguzi, vyombo vya dola na watoa taarifa kuwa wawazi na kutoa ushirikiano kwa vyombo vyote vya habari bila upendeleo.
Mwisho ZAMECO inatoa wito kwa waandishi wa habari na wadau wengine wa habari kuendelea kupaza sauti kudai upatikanaji wa Sheria Mpya ya Huduma za Habari Zanzibar na kuendelea kuwa mabalozi wa uhuru wa habari, uwajibikaji na uwazi katika jamii yetu.
“Kuwapo kwa Uhuru wa Habari ni chachu ya maendeleo katika nchi”
Post a Comment