MAADHIMISHO YA SIKU YA UHURU WA VYOMBO VYA HABARI DUNIANI KUFANYIKA MEI 17
NA MARYAM NASSOR
ZANZIBAR
Kamati ya Wataalamu wa Masuala ya Habari Zanzibar (ZAMECO) imesema Maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Habari Duniani yanategemewa kufanyika Jumamosi tarehe 17 Mei, 2025 katika ukumbi wa RAHALEO STUDIO kuanzia saa 2:30 asubuhi ambapo yatahudhuriwa na waandishi wa habari, wadau mbali mbali wa habari pamoja na wawakilishi kutoka taasisi za kiserikali na zisizo za kiserikali.
Makamo mwenyekiti wa kamati hiyo Dkt. Mzuri Issa amesema kuwa maadhimisho ya mwaka huu yana ujumbe muhimu na adhimu ambao ni “Sheria nzuri ya Habari ni chachu ya uchaguzi ulio huru na wa haki” Maadhimisho hayo ni muhimu katika kukuza na kuimarisha kada ya habari hapa nchini pamoja na kutoa wito maalum kwa wadau wa habari kuhusu umuhimu wa kuwa na Sheria mpya na rafiki yenye kusimamia mazingira salama kwa waandishi wa habari hasa kuelekea kipindi cha uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.
Aidha maadhimisho hayo yatatanguliwa na shughuli za kukuza na kuimarisha kada ya habari ikiwemo kuandaa vipindi vya masuala ya uhuru wa habari pamoja na mikutano na mafunzo kwa waandishi wa habari katika masuala ya sheria za habari. Pia kutakuwa na mjadala kuhusu nafasi ya wanawake katika vyombo vya habari na umuhimu wa usawa wa jinsia katika uongozi wa vyombo vya habari. “Nia ya shughuli hizo ni kukuza weledi na umahiri wa waandishi wa habari katika masuala ya sheria za habari ili watumie kalamu zao katika kufanya uchechemuzi wa sheria hizo, na suala la kufuata weledi na umahiri katika kada ya habari litahimizwa”.
Kutakuwa na mijadala inayohusu umuhimu wa Sheria Mpya ya Huduma za Habari
Zanzibar, Ulinzi kwa Waandishi wa habari wakati wa uchaguzi na haki ya kuripoti bila
kubaguliwa katika uchaguzi. Lengo ni kuimarisha na kukuza kada ya habari nchini yenye
kuleta maendeleo na kuibua kero za wananchi.
“Mijadala pia italenga katika kuandika habari za makundi ya pembezoni pamoja na
kunyanyua sauti za wasio na sauti” Makamo Mwenyekiti alifafanua Zaidi.
Kamati ya maadhimisho ya kuandaa Siku ya Uhuru wa Habari hapa Zanzibar (ZAMECO),
inaundwa na taasisi na wadau wa habari ikiwemo Baraza la Habari Tanzania Ofisi ya
Zanzibar (MCT ZNZ), Jukwaa la Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC-ZNZ)
Chama cha Waandshi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA, ZNZ) , Jumuiya ya Waandishi wa Habari za Maendeleo (WAHAMAZA) pamoja na Klabu ya Waandishi wa Habari Zanzibar.

Post a Comment