TAMWA ZNZ, ZAFELA NA PEGAO KUADHIMISHA SIKU YA MTOTO WA KIKE OKTOBA 17


CHAMA cha Wandishi wa Habari wanawake Tanzania Zanzibar, (TAMWA ZNZ)  kwa kushirikiana na jumuia ya wanasheria wanawake Zanzibar (ZAFELA) , jumuiya ya wanawake wenye ulemavu Zanzibar ( JUWAUZA) na Jumuiya ya Mazingira , Jinsia  na Utetezi Pemba, PEGAO, wataadhimisha  siku ya mtoto wa kike itakayo fanyika Alhamis, oktoba 17 ,2024, saa mbili za asubuhi  katika  ukumbi wa ZURA  Maisara  Unguja.

Katika maadhimisho hayo, kutakuwa na uwasilishaji wa tathmini ndogo ya kuangalia , nafasi za uongozi  kwa mtoto wa kike katika ngazi za skuli za msingi, sekondari na vyuo vikuu, tathimini  ambayo  itatoa mwanga wa kuweka kipaumbele kwa ajili ya kumuanda na kumnyanyua mtoto wa kike katika kushika nafasi za uongozi.

Hafla hiyo,itawashirikisha washiriki 70 wakiwemo, Watoto wenyewe, asasi za kiraia, taasisi za kiserikali na walimu ambapo ujumbe wa mwaka huu ni ‘ MUWEZESHE MTOTO WA KIKE, APAZE SAUTI YAKE’ wenye lengo la kuhimiza usawa wa kijinsia kwa kumpa mtoto wa kike fursa sawa za uongozi katika ngazi za awali ili aweze kufikia  ndoto zake bila vikwazo vyovyote.

Pamoja na mikakati inayotekelezwa  na wadau mbali mbali, Watoto wakike bado wanakumbana na changamoto  nyingi zikiwemo udhalilishaji , kutopewa fursa  sawa na Watoto wa kiume, na mitazamo hasi  ya kiutamaduni inaowanyima haki  za msingi zikiwemo nafasi za uongozi.

 Aidha, siku ya Mtoto wa kike Duniani huadhimishwa oktoba 11 kila mwaka. Siku hii ilianzishwa na umoja wa mataifa mwaka 2012 ili kuangazia haki za wasichana  na changamoto wanazokumbana nazo dunini kote, lengo lake ni kuhamasisha juhudi za kuboresha fursa za elimu, Afya , Ulinzi na usawa  wa kijinsia  kwa wasichana na kuhimiza wadau kuhakikisha wanatatua changamoto  zinazomkwamisha mtoto wa kike kufikia ndoto zake hasa katika uongozi.              

                               MWISHO

 

No comments

Powered by Blogger.