WANAFUNZI CHUO CHA IPAA PEMBA WATAKA KUTATULIWA CHANGAMOTO ZAO ZINAZOWAKABILI
NA MARYAM NASSOR Pemba,
UONGOZI wa serikali ya wanafunzi chuo cha utawala wa umma Zanzibar ,(IPA) tawi la Pemba wamewataka Viongozi wa chuo hicho kutatua changamoto zinazowakabili kwa wakati.
Ombi hilo, limetolewa na naibu waziri mkuu wa Serikali ya wanafunzi, Pemba,Rashid Khamis Yussuf mara baada ya kuapishwa na kupata cheo hicho huko mjini Chake chake .
Alisema ,chuo hicho kinakabiliwa na changamoto lukuki ambazo zinashindwa kupatiwa ufumbuzi kwa wakati sahihi.
Alisema kuwa,kuna kipindi walikuwa na shida ya maji katika chuo hicho, na shida hiyo ilidumu kwa muda mrefu na muhasibu alishindwa kuchukuwa pesa ili kulitatua tatizo hilo .
“Kuna wakati tulikuwa na shida ya maji katika chuo chetu, na tatizo hilo lilidumu kwa muda, bila ya kupatiwa ufumbuzi na muhasibu yupo lakini alishindwa kulishuhulikia”alisema.
Mwanafunzi Deo Mabula Alfred, alisema yeye changamoto inayomkera ni kutokupewa vitambulisho, kile cha mitihani na cha wanafunzi kwani walishakutana na tatizo la kutolewa kwenye mashindano ya bonaza, tu kwa sababu hawana kitambulisho.
“Kuna siku nusra tupigane kwenye bonaza la zayadesa, tushacheza mpira bado kidogo tuondokee na mbuzi, tukatolewa kwenye mashindano kwasababu hatuna vitambulisho vya chuo”alisema.
Alisema kuwa, pia vyeti vya kumalizia masomo hawapewi kwa wakati kwani kuna wanafunzi wameshaingia ngazi ya diploma lakini vyeti vyao hawajavipata.
Nae, mwanafunzi Ali Mohamed Omar, alisema kuwa tokea ajiunge na chuo hicho, ni mwaka mmoja na nusu sasa,hawajapatiwa hata elimu ya majanga kama moto na ndani ya chuo mitungi ya kesi yakuzimia moto yapo.
Alieleza kuwa,hata huduma ya kwanza hawajawahi kufundishwa na wanakaa wanafunzi wengi na kila mtu na maradhi yake , ikitokea mwanafunzi mmoja , kakutwa na majanga, basi watashindwa kumsaidia .
Nae, Rais wa Serikali ya wanafunzi wa chuo hicho, Nagila Abdallah Ali akijibu maswala ya wanafunzi hao alisema kuwa, yeye ni Rais mwanamke wa kwanza katika chuo hicho tokea kianzishwe.
Alisema kuwa,yeye kaja Pemba ili kuja kuwapisha viongozi wapya na kutatua changamoto za wanafunzi zinazowakabili na asizo ziweza atazichukuwa kuzipeleka kunako husika.
Aidha alisema kuwa,viongozi hao waliochaguliwa wafuate njayo za viongozi waliyopita kabla yao, huku akimtolea mfano aliyekuwa waziri wa mikopo aliyepita alikuwa na mashirikiano mazuri na viongozi wenzake.
Aliwataka , viongozi waliyochaguliwa kutoa mashirikiano mazuri na kutatua shida zitakazowakumba wanafunzi wakiwa wanaendelea na masomo chuoni hapo.
Awali Rais huyo wa Serikali ya wanafunzi, aligawa zawadi ya pedi kwa wanafunzi wa kike wa chuo hicho kama shukrani ya kuchaguwa kwake na kuwataka viongozi hao waliyochaguliwa kuwa tayari kwa safari ya kwenda unguja kwa ajili ya kupatiwa mafunzo ya uongozi.
Katika hafla hiyo, waliapishwa viongozi mbali mbali akiwemo, Naibu waziri mkuu wa Serikali ya wanafunzi, waziri wa afya na mazingira, waziri wa elimu na waziri wa michezo ambapo mawaziri wawili walikuwa ni wanawake.
MWISHO