TAMWA ZNZ YAISHAURI SERIKALI KUJA NA KANZI DATA AMBAYO ITAONESHA WANAWAKE WANGAPI WAPO KWENYE SEKTA YA UONGOZI NCHINI
NA MARYAM NASSOR,
CHAMA cha Wandishi wa habari wanawake Zanzibar (Tamwa) kimeishauri Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, kuanzisha kanzi data za kitaifa ambazo zitaonesha idadi ya viongozi wanawake ambao wako katika sekta mbali mbali za uongozi nchini.
Ushauri huo umetolewa, na mkurugenzi wa Tamwa Zanzibar dk Mzuri Issa huko katika ofisi za Tamwa Tunguu, alipokuwa akizungumza na wandishi wa habari hizi,juu ya mafanikio yaliyofikiwa katika mradi wa kuwawezesha wanawake na jamii kudai haki zao za kidemokrasia na uongozi.
Alisema , Zanzibar hakuna kanzi data ambazo zinaonesha moja kwa moja, kuwa kuna wanawake wangapi katika sekta mbali mbali za uongozi nchini, hivyo inakuwa ni vigumu kujua tathimini yao.
‘’Hatuwezi kusema kwa uhakika, kuwa kuna viongozi wanawake wangapi katika sekta mbali mbali nchini,kwasababu hatuna kanzi data ambazo zinaonesha idadi yao’’ alisema.
Aidha alisema kuwa, serikali inatakiwa kuwa na sera madhubuti ambazo zitalazimisha usawa wa kijinsia katika sekta zote za uongozi nchini na mifumo rafiki kwa upatikanaji wa haki kwa wananchi wote.
Akijibu baadhi ya maswali ya wandishi wa habari, mratibu wa chama cha wandishi wa habari wanawake kwa upande wa Pemba, Fathiya Mussa Said alisema, wana chukuwa hatua kubwa ya kufanya uchechemuzi kwa wanawake kwasababu hata katika dini imemtaaja mwanaume kuwa ni kiongozi, hivyo inakuwa ni rahisi kwao kuingia kwenye uongozi.
Hivyo,wanafanya ushawishi mkubwa kwa wanawake ili kuwajengea uwezo wa kujiamini na kuwa rahisi kwao kugombania nafasi mbali mbali za uongozi ili kujiletea maendeleo.
Nao, baadhi ya wandishi wa habari waliyopata nafasi ya kuliza maswali ,waliuliza kuwa, hiyo nguvu inayotumika kuwashajihisha wanawake katika uongozi mbona, haitumiki kwa upande wa wanaume.
Akijibu maswali hayo, mkurugenzi wa pegao Pemba, Hafidh Abdi Said alisema kuwa, nguvu nyingi inatumika katika kumnyanyua mwanamke kwa sababu hapo, awali alikuwa hana iyo nafasi.
Alisema, mwanamke ukimpa nguvu anaweza kujifunza na kudai haki zao za kidemokrasia na uongozi, kwani wanaamini ukimuelimisha mwanamke mmoja basi umeielimisha jamii nzima,
Mkurugenzi huyo, wa pegao Pemba,aliwatoa wasi wasi wanaume ambao wanania ya kuwania nafasi za uongozi, kwani muda ukifika kitakachoangaliwa ni yupi mtu sahihi ambae anafaa kuwa kiongozi haitaangaliwa jinsia yake.
Aidha alisema kuwa, licha ya kumalizika kwa mradi huo wa (SWIL) ambao uliolenga kumuwezesha mwanamke, siyo tu kuwa kiongozi bali kuwa kiongozi bora, lakini uchechemuzi utaendelea, kwani kuna wahamasishaji jamii ambao wataendelea kutoa elimu.
Mradi huo wa kumuwezesha mwanamke na jamii kudai haki zao za kidemokrasia na uongozi (SWIL) ulianza mwaka 2020 hadi kumalizika mwaka jana 2023, wakishirikiana na jumuiya ya wanasheria wanawake Zanzibar, Zafela pamoja na jumuiya ya utetezi na uchechemuzi wa jinsia na mazingira Pemba, Pegao na Tamwa Znz na kufadhiliwa na ubalozi wa Norway nchini Tanzania ambao umepata mafanikio mbali mbali hadi kumalizika kwake.
Post a Comment